MICHEZO


 NGASA KUCHEZA YANGA NA KUILIPA SIMBA 45MILLION
 Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imepitia usajili wa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom na kumuidhinisha Mrisho Ngasa kuchezea timu ya Yanga baada ya kukamilisha usajili wake.
Hata hivyo, Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa imebaini kuwa Ngasa alisaini mkataba mwingine Simba (katika kipindi ambacho alikuwa na mkataba na Azam) ambapo anatakiwa kurejesha fedha alizopokea (sh. milioni 30) pamoja na fidia ya asilimia 50 (sh. milioni 15) ya fedha hizo kwa Simba.
Kamati pia imemfungia mechi sita za mashindano (kuanzia mechi ya Ngao ya Jamii), na anatakiwa awe amelipa fedha hizo ndani ya kipindi hicho cha kukosa mechi hizo. Akishindwa, hataruhusiwa kucheza hadi atakapolipa fedha hizo.
Vilevile Kamati imepitia pingamizi zote zilizowasilishwa kuhusu usajili wa wachezaji, kukatiza mikataba ya wachezaji na kuzitaka klabu husika ziwe zimetatua masuala hayo hadi Alhamisi (Agosti 22 mwaka huu).
Kwa upande wa wachezaji wa kigeni, Kamati imeagiza wasiruhusiwe kucheza hadi watakapopata Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC) pamoja na vibali vya kufanya kazi nchini (work permits).
Kamati hiyo itakutana tena Ijumaa (Agosti 23 mwaka huu) ili kupata ripoti za pingamizi ilizoagiza ziwe zimefanyiwa kazi hadi Agosti 22 mwaka huu na kutoa uamuzi kwa pande ambazo hazikuafikiana.


  LUIS SUAREZ KAAMUA KUBAKI LIVERPOOL
Mshambuliaji Luis Suarez amesema hafikirii tena kuondoka Liverpool, na kwamba anabaki kwa sababu ya heshima ya mashabiki wa timu hiyo.
London, England. Luis Suarez kwa mara ya kwanza amesema ameamua kubaki Liverpool na sababu kubwa ya uamuzi huyo ni mashabiki wa Uwanja wa Anfield.
Nyota huyo wa kimataifa kutoka Uruguay, kwa muda mrefu amekuwa akishikilia msimamo wake wa kutaka auzwe.
Klabu ya Arsenal ilikuja na ofa mbili tofauti na zote zilikataliwa Anfield, huku klabu yake mara zote ikisisitiza kutouzwa mchezaji huyo.
Arsenal ilituma ofa ya Pauni 40 milioni, kisha ikatuma nyingine ya Pauni 41 milioni. Hazikukubaliwa Anfield.
Lakini sasa, Suarez amekubaliana na msimamo wa viongozi wake na kusema anabaki Anfield.
Aliyaambia magazeti ya Uruguay: “Kwa sasa sifikirii tena kuondoka, na hii ni kutokana na hisia za watu wengi kwangu.”
Kwa sasa Suarez yuko na timu ya Taifa ya Uruguay.
Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers alimtaka Suarez kufanya mazoezi peke yake, wakati kikosi chake kikiwa kwenye mechi za maandalizi ya msimu wa Ligi Kuu England unaoanza mwishoni mwa wiki hii.
Kocha wa Liverpool mbali na kumtaka Suarez kufanya mazoezi peke yake, pia alimtaka kuomba radhi kutokana na kauli alizokuwa akizitoa mara kwa mara kuhusu kutaka kuondoka.
Hata hivyo, Suarez atakosa mechi sita za mwanzo ligi kuu kwa kutokana na kutumikia adhabu kwa kosa la kumng’ata meno beki wa ChelseaBranislav Ivanovic msimu uliopita.

No comments: